Thursday 28 May 2015

SILAHA NANE ZA KUFUNGUA MILANGO NA MALANGO YALIYOFUNGWA MBELE YAKO;

SILAHA YA TATU

USIKATE TAMAA
Usikate tamaa katika yale unayo yaamini BWANA atakufanyia, kwakuwa Mungu wetu hachelewi wala hawai isipokuwa anajibu kwa wakati wake. Maisha ya imani yanahitaji mtu mwenye moyo imara katika Kristo Yesu asiye yumba wala kutetemeshwa. Pia yatupasa tufahamu kipo kipindi ambacho imani inaweza kutindika, panahitajika maombi yenye kuinua imani. Maombi haya aliyafanya Yesu kwa Petro ili imani ya Petro isitindike; “Akasema, Simon, Simon, tazama, shetani amewataka nyinyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka uwaimarishe ndugu zako.” Luka 22:31-32
Malango na Milango yatafunguka pale Mhitaji au Mwombaji atakapo mwomba Mungu aliye hai pasipo kukata tamaa. Maana maombi endelevu uleta ushindi na baraka endelevu. Silaha hii ya tatu ni ya muhimu sana kwa mtu wa Mungu. Bwana Yesu kristo anathibitisha; “Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumuomba Mungu siku zote, wala msikate tamaa. Akasema palikua na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa, halafu akasema moyoni mwake, ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini kwakuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia atawapatia haki upesi; walakiniatakapokuja mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” Luka 18:1-8

Na Mungu je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku naye ni mvumilivu kwao. Nawaambia atawapatia haki upesi lakini atakapokuja mwana wa Adamu je ataiona Imani duniani? Bwana Yesu Kristo aliuliza swali hili kwa lengo la kuwajenga wanafunzi wake wasikate tamaa kamwe, wakati wa kuinuliwa ukifika watainuliwa tu. Maana nyakati za kuburudishwa zimewadia sharti upate kuburudishwa katika BWANA. Sawasawa na Neno la Mungu lililonenwa katika kinywa cha nabii Isaya; “Nyakati zako zitakua ni nyakati za kukaa imara; za Wokovu tele na Hekima na Maarifa. Kumcha BWANA ni hazina yake ya akiba.” Isaya 33:6

Ndani mwa Maombi haya; ukiomba na kumsihi Mungu pasipo kukata tamaa, yeye atakuinua na atazifanya nyakati zako kuwa nyakati za kukaa imara Kiroho na Kimwili. Maana Malango yako ya Kiuchumi yatakuwa Imara, Kazi ya Mikono yako haitazaa kufakufa wala kuzaa mapooza. “Watu wa mjini wakamwambia Elisha, angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama BWANA wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. Akasema, nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, nimeyaponya maji haya, hakutatoka huko tana kufa wala kuzaa mapooza. Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.” 2 Wafalme 2:19-22

Kukata tamaa kulimfanya Musa apishane na uponyaji wake. Mungu alikusudia kumponya Musa kigugumizi lakini Musa akawa mkata tamaa maana aliona amezaliwa hivyo, hivyo hawezi kupona. Maandiko matakatifu yanathibitisha; “Musa akamwambia BWANA, Ee Bwana, mimi si msemaji tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako, maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona au kuwa kipofu? Si mimi BWANA? Basi sasa enenda nitakuwa pamoja na kinywa chako, kukufundisha utakalolinena. Akasema, Ee Bwana nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema je! Hayuko Haruni ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo tazama, anakuja kukulaki naye atakapokuona atafurahi moyoni mwake. Nawe utasema naye, nakuyatia maneno kinywani mwake, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako na pamoja na kinywa chake na kuwafundisheni mtakayofanya. Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi  mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara.” Kutoka 4:10-17

Bwana anamwambia Musa; Je aliyeumba kinywa cha binadamu ni nani?, Je ni nani aliyemfanya mtu kuwa bubu?, Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi? Na ni nani aliyemfanya mtu awe mwenye kuona? Bwana anamwambia Musa nenda, ntakuwa na kinywa chako, nitakufanya upate kusema vema lakini Musa akasema; Mungu, tuma mtu mwingine, HASIRA YA BWANA ikawaka juu ya Musa ndipo akamuacha akamtuma Haruni. Mahali hapa tumejifunza jambo la msingi ambalo Mungu halipendi ni kukata tamaa. Milango na Malango yatafunguliwa kwa Imani thabiti sio kwa Imani ya kukata tamaa.

Kwa Imani, Malango yote yaliyofungwa sharti yafunguliwe. Kristo amekusudia kututendea mema katika maisha yetu, hakuna atakayezuia maana hakuna awezaye kulizuia kusudi la Mungu kwako. Simama Imara usikate tamaa wala usife moyo. BWANA anasema katika kinywa cha nabii Isaya: “Maana BWANA wa Majeshi amekusudia naye ni nani atakayelibatilisha? Na Mkono wake ulionyoshwa ni nani atakayegeuza nyuma?” Isaya 14:27

GIDION alikata tamaa kutokana na ugumu wa maisha waliokuwa wanapitia kama Taifa, Lakini Israeli alipomlilia BWANA, akamuinua Gidion katika hali ile ya kukata tamaa, akainuliwa roho yake na kufanyika mlango wa ukombozi kwa wana wa Israeli dhidi ya majeshi ya Wamidiani. Japo yeye alijiona maskini asiyeweza kutokana na udogo wa kabila lake lakini kwa imani katika Mungu, aliwapiga Wamidiani kama mtu mmoja. Maandiko yanathibitisha;  “Kisha wana wa Israel walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA; BWANA akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba, mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki wakakwea juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo wala ng’ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng’ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani, nao wana wa Israeli wakamlilia BWANA. Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia BWANA kwa sababu ya Midiani, BWANA akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli, naye akawaambia, BWANA yeye Mungu wa Israeli asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa; nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao kisha niliwaambia, Mimi ndimi BWANA Mungu wenu, msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao lakini hamkuitii sauti yangu. Malaika wa BWANA akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri na mwana wa Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo ili kuificha machoni pa Wamidiani. Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia, BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa, Gideoni akamwambia Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyo tuhadithia baba zetu, wakisema, je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. BWANA akamtazama, akasema, enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kwa mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninaye kutuma? Akamwambia, Ee Bwana nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. BWANA akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.” Waamuzi 6:1-16

Yako mambo mengi ya kukatisha tamaa lakini katika Kristo Yesu upo mlango wa kutokea. Usife moyo bali jitie nguvu katika BWANA. Maombi ya wana wa Israeli yalifungua Malango na Milango wakainuka tena. Nawe waweza kuinuka tena maana ni tabia ya Mungu isiyobadilika kuwainua watu wake wanaomlilia mchana na usiku. Maana maandiko yanathibitisha katika kitabu cha 1Samweli 1:6-9 “BWANA huua, naye hufanya kuwa hai; hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. BWANA hufukarisha mtu, naye hutajirisha; hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, humpandisha mwitaji kutoka jaani, ili awaketishe pamoja na wakuu, wakirithi kiti cha enzi cha utukufu. Kwa maana nguzo za dunia zina BWANA, naye ameuweka ulimwengu juu yake. Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; bali waovu watanyamazishwa gizani, maana kwa nguvu hakuna atakaye shinda.” 

Angalia Bathromayo mwana wa Timayo, yule kipofu wa kuzaliwa; Alikatishwa tama wakati alipokuwa anamwita Yesu lakini yeye hakukata tamaa bali aliendelea Kuomba, akapaza sauti yake kwa nguvu naye Yesu akamwitikia na kumfungua. “Wakafika Yeriko, hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake na kusema, mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema mwiteni. Wakamwita Yule kipofu, wakamwambia, jipe moyo, inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.” Marko 10:46-52

Naipenda imani ya Bartimayo kwa kuwa hakujidharau japo watu walimdharau, walimwona hafai (rejected man). Mwana wa Mungu katika maisha yako utakutana na watu wenye dharau, kebehi, viburi, waliojaa masimango na vinywa vya ukaidi. Wataipepeta imani yako kwa maneno yao ili utindikiwe kiimani, lakini nakutia moyo, vuka mipaka utakayowekewa mbele yako (GO BEYOND YOUR LIMITATIONS). Wengi; Watakubeza, Watakusemasema, Watakudharau; Wewe simama katika Imani yako wala usikate tamaa, Mlango wa Uzima utafunguliwa na Lango la Baraka litafunguliwa.

Mkuu wa Sinagogi alipokea ufufuo wa mtoto wake aliyekuwa amekufa wakati amemfuata Yesu aje amponye huku nyuma mtoto akafariki na taarifa ikaja ikisema, usimsumbue mwalimu mtoto amekwisha kufa.

“Hata Yesu alipokwisha kuvuka kurudia ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye, mkutano mkuu wakamfuata, wakamsonga-songa… hata alipokuwa katika kunena wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, binti yako amekwishakufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, aliposikia lile neon likinenwa akamwambia mkuu wa sinagogi, usiogope, amini tu… wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia akawaambia, mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. WAKAMCHEKA SANA. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote akamtwaa babaye Yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, thalita, kumi; tafsiri yake, mschana, nakwambia inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. MARA WAKAMSHANGAA MSHANGAO MKUU. Akawaonya sana mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.” Marko 5:21-24, 35-43 

Pata picha hapa ya kutokukata tamaa; Huyu mkuu wa sinagogi amemuacha mtoto anaumwa nyumbani kwake, anamfuata Yesu aje amponye, anakwenda kwenye maombi ghafla analetewa habari mbaya na ngumu yakuwa mtoto wake amekwisha kufa achana na maombi. Lakini hata aliporudi nyumbani mwake na Kristo Yesu, alipokelewa na msiba na maombolezo makuu, bado maombolezo makuu hayakugeuza imani yake kwa Kristo, aliendelea kuamini Neno la Kristo Yesu. Neno la BWANA linasema; “Msiyakumbuke mambo kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito nyikani.” Isaya 43:18-19
Waombolezaji hawakuhitaji imani ili kuomboleza bali Yairo mkuu wa sinagogi alihitaji imani thabiti ili binti yake afufuliwe. Yesu Kristo anasema binti amelala wakati waombolezaji wao wanasema kafa, ndio maana walimcheka sana kwa kuwa aliongea kitu kilichozidi ufahamu na akili za waombolezaji. Ili mtu wa Mungu asikate tamaa anahitaji kuwa na imani iliyo juu zaidi ya akili za wanadamu, maana njia za Mungu hazichunguziki na makusudi yake hayawezi kuzuilika.  

“Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa, uwaage watu hawa ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula. Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula? Akawaambia mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, mitano na samaki wawili. Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi. Wakaketi safusafu, hapa mia hapa hamsini. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie na wale samaki wawili akawagawia wote. Wakala wote wakashiba. Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili na vipande vya samaki pia.” Marko  35-43

Inawezekana nawe umezoea kupokelewa na Misiba mwaka kwa mwaka nyumbani mwako. Unapokelewa na Magonjwa mwaka kwa mwaka uzao hadi uzao, Unapokelewa mwaka kwa mwaka na Kufeli katika Masomo. Usiogope, Amini tu katika Kristo kwani yote yanawezekana kwake yeye aaminiye tu na si vinginevyo. “yote yawezekana kwake aaminiye.” Marko 9:23

Maandiko matakatifu yanatujenga kiimani yakuwa tusiogope habari mbaya zijapo bali tujithibitishe katika imani mpaka tutakapoona watesi wetu wameshindwa na kuwekwa chini ya miguu yetu, sawasawa na Neno la Mungu katika Zaburi 112:7-8
 “Hataogopa habari mbaya, moyo wake u Imara ukimtumaini BWANA; Moyo wake umethibitika hataogopa, HATA AWAONE WATESI WAKE WAMESHINDWA.”

“MJANE WA SEREPTA”
Angalia Mjane huyu wa Sarepta akiwa katika hali ya kukata tamaa, hana kitu lakini alipotii Neno la Mungu, hakika Mungu aligeuza Masikitiko yake kuwa Furaha. Mjane huyu akiwa anaomba katika hali ngumu, BWANA akamtuma Nabii Eliya alete jibu; “Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, niletee nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, niletee nakuomba kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana Mungu wako aiishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokata kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Elia akamwambia, usiogope, enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee, kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwakuwa BWANA, Mungu wa Israel, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; nayeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya.” 1Wafalme 17:8-16

Mjane, anaombwa atengeneze mkate kwa ajili ya Nabii naye akasema; “Kama BWANA Mungu aishivyo, sina mkate ila konzi ya unga katika pipa na mafuta kidogo katika chupa nami naokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tule tukafe.” Imani ya Mama huyu mjane ilikuwa  imefika mwisho, alikuwa hana matumaini tena ya kuishi kutokana na hali halisi ilivyokuwa katika nchi yake na katika mazingira aliyokuwemo. Ndivyo wakristo wengi walivyo leo, japo wanasali lakini hawana matumaini tena kutokana na mapito yao wanayopitia. Na wengi wamepishana na Miujiza yao na Malango yao ya Baraka yameendelea kufungwa kwa sababu ya kukata tamaa.

Wakristo wengi wanataka kuona miujiza ikitendeka pasipo wao kuamini kwanza ndipo miujiza itendeke. Wengi wanashindwa kutoa zaka kamili mbele za Mungu aliye hai kwasababu ya ugumu wa maisha. Bwana anasema lete zaka kamili, wewe unatoa nusu au hutoi kabisa, Malango yako na Milango itaendelea kufungwa tu mpaka utakapolitii Neno la Mungu. Ndiyo maana nabii Eliya mtishibi alitaka mjane huyu atii agizo la Mungu kwanza la kutengeneza mkate bila kujali kitakachobakia kwenye pipa lake la unga na kwenye chupa yake ya mafuta. Lakini jambo la ajabu la ki-Mungu kila alipochota unga haukwisha na kila alivyomimina mafuta hayakuisha mpaka njaa ilipokoma. Hivyo mtumishi mwaminifu atastawi daima katika nyua za BWANA. Fahamuni ndugu zangu Mungu hana kigeugeu akisema iwe inakuwa, akisema ndiyo ni ndiyo. “Kwa kuwa mimi BWANA, sina kigeugeu, ndiyo maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo. Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, name nitawarudia ninyi, asema BWANA wa Majeshi. Lakini ninyi mwasema turudi kwa namna gani? Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu, ninyi mmelaaniwa kwa laana kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni Baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwaajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi. Na mataifa yote watawiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema BWANA wa majeshi.” Malaki 3:6-12

Pili, Acha kujidharau wala usidharau ulichonacho, Mungu aliye hai yeye atafanya njia mahali pasipo kuwa na njia, ndiyo kazi yake. Eliya Nabii akamwambia Mjane, Usiogope, nenda uakanifanyie mkate, kwanza ukaniletee nile ndipo ujifanyie wewe na mwanao.
“Kwa kuwa Bwana Mungu wa Israeli asema hivi lile pipa la unga halitapunguka wala ile chupa ya mafuta haitaisha hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.” Mjane yule akafanya kama mtumishi wa Mungu Eliya alivyosema; Maana yake aliamini na kukata tamaa kukaondoka, hakika aliona maajabu. Usikate tamaa, Yesu Kristo yupo atakufungulia Malango na Milango yako; Amesema, atatenda tu maana kwa kusudi hili amedhihirishwa ili azivunje kazi za Ibilisi. Piga mbio katika Maombi, majibu yako yapo.

Dada huyu aliambiwa Hospital kuwa hatazaa kwasababu tumbo lake limejaa mauvimbe makubwa ambalo lazima afanyiwe upasuaji atolewe kizazi; lakini tarehe 04/08/2013, aliponijia akanieleza yaliyompata ndipo nikamwambia “Usiogope, Kuzaa utazaa maana Kristo atafanya njia mahali pasipo kuwa na njia” Nikampa andiko; 
“Akajibu akasema, kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbunguni, litang’olewa.” Mathayo 15:13

Baada ya hapo, nikamfanyia Maombi, mwezi uliofuata akapata mimba, akaendelea kuja kwenye maombi maana nilimueleza mfano wa kuku wa kienyeji, anapotaka kutotoa vifaranga utamkuta masaa yote amelala juu ya mayai yake mpaka siku ile anapototoa vifaranga vyake. Nawe kaa kwenye Maombi, naye kweli alikaa kwenye maombi; Mpaka anakwenda kujifungua, anasema Mchungaji Niombee maombi, sasa amepata mtoto wa kike anaitwa Sarah na tarehe 25/05/2013 tulimbariki huyu mtoto akiwa na siku 14 tu tangu azaliwe; Jina la Bwana Libarikiwe.




2 comments:

  1. Amina mtumishi wa Bwana umeniponya na malango na milango imefunguka sasa

    ReplyDelete
  2. Amina mtumishi wa Bwana umeniponya na malango na milango imefunguka sasa

    ReplyDelete

Total Pageviews

Eagt City Centre Blog 2013. Powered by Blogger.

About Me

My photo
Jicho langu latoka machozi lisokome,wala haliachi;Hata BWANA atakapoangalia. Nakutazama toka mbinguni Maombolezo 3:49-50

Followers

Featured Posts

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget